FEISAL SALUM ABDALLAH (Fey Toto) NI MCHEZAJI MWENYE KIPAJI CHA MPIRA WA KUZALIWA..
- Simon Kimanga
- 2024-03-23
FEISAL SALUM ABDALLAH (Fey Toto) NI MCHEZAJI MWENYE KIPAJI CHA MPIRA WA KUZALIWA..
- Simon Kimanga
- 2024-03-23
Uwekezaji wa Bandari ya Dar Es Salaam – bado hakieleweki. |
Dar es Salaam. Hakuna
unachoweza kusema zaidi ya kueleza kuwa suala la bandari limeendelea kuwa na
mitazamo na misimamo tofauti.
Wakati jana Kamati Kuu
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiweka bayana msimamo wake kwa
umma wa kupinga mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari
nchini kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, jana hiyohiyo, Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliongoza timu ya wataalamu
walioshughulikia mkataba huo kutoa elimu kwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
akitetea uwekezaji huo, sambamba na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas
Ndumbaro ambaye naye alilizungumzia.
Mbali na wote hao,
Rais Samia Suluhu Hassan alitumia sehemu ya hotuba yake fupi Ikulu ya Dar es
Salaam, wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni,
kuelezea umuhimu wa kuchangamkia fursa ikiwemo hiyo ya uwekezaji bandarini na
kuzilinda.
Katika maelezo yake,
Rais Samia alisema: “…hili la fursa, nataka niseme vizuri, wakati sisi
tunalumbana, bandari apewe nani, iende, isiende, ikae, wenzetu kwa kuona
malumbano yetu, wameruka, wamekwenda kulekule na lilelile jumba lililowekwa
bendera ya Tanzania limeweka bendera ya jirani, sasa Tanzania tumeuza wale
jirani wamekimbilia kule wemekwenda kufanya nini?”
Rais aliongeza: ‘‘Siku
ileile Bunge linaridhia azimio la kukubali ushirikiano, siku ya pili wakasema
ninyi bandari moja, sisi zote na wakakimbia kuwahi nafasi, sasa muone jinsi
fursa zinavyokuja na kukimbia harakaharaka.”
Licha ya Rais Samia
kutobainisha jina la jirani wala hilo jumba, lakini alikuwa akimaanisha ni nchi
ya Kenya ambayo rangi ya bendera yake ilipambwa kwenye mnara wa Burj Khalifa
uliopo Dubai, kama ilivyokuwa kwa rangi ya bendera ya Tanzania iliyowahi
kupambwa kwenye mnara huo.
Si kauli ya kwanza kwa
Rais Samia kuhusu suala hilo kwani Juni 13 mwaka huu, mara tu baada ya kuwasili
jijini Mwanza kuanza ziara aligusia akisema atafanya kila analoweza kufanya
Tanzania iendelee.
“Tanzania ni moja,
haigawanyiki wala haiuziki. Kwa hiyo ndugu zangu mama ni Mtanzania, maendeleo
yetu ndiyo muhimu, kila linalofanyika ni kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,”
alisema.
Mbarawa na wahariri
Waziri Mbarawa
aliongoza timu ya wataalamu mbalimbali wa wizara yake ya ujenzi na uchukuzi
akiwemo Hamza Johari, aliyeongoza timu ya majadiliano ya mkataba huo wa
uwekezaji kuzungumza na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Katika mkutano huo ulioanza
saa 4 asubuhi na kumalizika saa 8 mchana huku ukirushwa moja kwa moja na vyombo
vya habari ambapo wahariri walipata fursa ya kuwasikiliza wataalamu pamoja na
kuuliza maswali.
Johari alisema
uwekezaji utakaofanywa na kampuni ya DP World, ni asilimia nane pekee ya
shughuli zote zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TPA).
Hamza ambaye pia ni
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) alisema kutokana
na ufinyu huo wa uwekezaji, ndio maana Zanzibar na bandari zingine ikiwemo ya
Mtwara haikutajwa kwenye mkataba huo.
Alisema DP World
haitakuwa na haki ya kumiliki ardhi ya Tanzania kama inavyosemwa, bali maeneo
yote itakayofanyia kazi itakodishiwa na si kumilikishwa.
Hamza ambaye ni
kitaluma ni mwanasheria wa sheria za kimataifa, alisema kampuni hiyo
itakapokuja kuwekeza nchini lazima isajiliwe Tanzania na asilimia 35 ya
wafanyakazi wake watakuwa ni Watanzania.
“Ni kama ilivyokuwa
Ticts (Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania), atatoa
hisa kwa Watanzania, pia atalipa kodi na asilimia 35 ya wafanyakazi ni wazawa,
kwa hiyo DP World hawawezi kuja nchini mzima mzima,” alisema na kuongeza:
“Mkataba huu wa ushirikiano hauna shida yoyote na ninaposikia watu wanazungumza
nasikitika sana.”
Kuhusu maoni yaliyotolewa
na Mwanazuoni nguli, Profesa Issa Shivji, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
na wadau mbalimbali kuhusu mkataba huo, Serikali ilisema itafanyia kazi kwenye
mikataba ya kibiashara itakayosainiwa baina ya TPA na DP World.
Mwanasheria wa Wizara
ya Ujenzi na Uchukuzi, Mohamed Salum alisema asilimia 80 hadi 90 ya maoni
yaliyotolewa kuhusu mkataba huo, yamegusa mikataba midogomidogo ambayo maoni
hayo yatazingatiwa kabla ya kusainiwa.
“Kama Serikali
tutachambua maoni ya TLS tukiona kuna vipengele vitaathiri utekelezaji wa huo
mkataba wa biashara, tutakwenda kwenye mabadiliko kwa mujibu wa ibara ya 22,”
alisema
Kuhusu maoni Profesa
Shivji, Salim alisema mwanazuoni huyo alichambua vyema mkataba huo hasa
akigusia kuwa mkataba huo ni wa upande mmoja.
Alisema ipo tofauti
kubwa kati ya BIT na IGA.
Yaani mkataba wa BIT
na IGA akifafanua kwamba BIT ni mkataba wa jumla baina ya nchi na nchi kuvutia
wawekezaji baina ya nchi nan chi,
Salim alisema
IGA inagusa mkataba mahususi kwenye mradi, hivyo kwa kuwa eneo la bandari ya
Tanzania ndio uwekezaji unafanyika lazima haki itolewe kwa DP World na Tanzania
iwe na wajibu.
“Mkataba huu hautoi
haki kwamba Tanzania ikawekeze Dubai, ingekuwa BIT ingekuwa na taswira ya jumla
tunazungumza haki na wajibu wa Tanzania, haki na wajibu alizozungumza Profesa
Shivji yupo sahihi lakini kwa sababu hii IGA, inatoa hakikisho kwa Serikali ya
Dubai kwa uwekezaji utakaofanya Tanzania,” alisema
Kwa upande wake,
Waziri Mbarawa alisema kwa sasa bandari ya Dar es Salaam inachangia asilimia 37
kwenye pato la Taifa na endapo uwekezaji huo utafanikiwa utachangia asilimia
67.
"Tuna jukumu
kubwa kwas ababu nyote mnajua Serikali inajenga miradi mikubwa na hatutaendelea
kila siku kupeleka bakuli kuomba omba wakati tuna rasilimali ambayo tukiitumia
vizuri na kuendesha vizuri, tutaweza kubadilisha uchumi wa Tanzania,"
alisema.
Msimamo wa Chadema
Jana hiyohiyo,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikutana na waandishi wa habari kutoa
maazimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyokutana Julai 8 mwaka huu kuhusu
suala hilo pekee na mengine akisema yatatolewa wakati mwingine.
Kutokana na maazimio
hayo, operesheni ya chama hicho ya '+255 Katiba Mpya' kwa sasa itajulikana kama
'+255 Katiba Mpya, Okoa Bandari Zetu.”
Operesheni +255 Katiba
Mpya ilizinduliwa Mei 17, mwaka huu mkoani Kigoma ikilenga kikuhuisha chama
hicho kuanzia ngazi ya chini na kuhamasisha umma juu ya kuidai Katiba Mpya.
Awamu ya pili ya operesheni hiyo itazinduliwa Julai 28, mwaka huu.
Mabadiliko ya
operesheni hiyo ni miongoni mwa maazimio ya Kamati Kuu hya Chadema na kwamba
wataizindua mkoani Kagera na kuendelea katika mikoa ya Geita, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu na Mara.
"Tunakusudia
kuifanya nchi nzima na itazinduliwa kwa kwenda kutangaza namna CCM na Serikali
yake inavyoharibu nchi kwa mikataba isiyo na tija kwa kizazi cha leo, kesho na
keshokutwa.
“Tumesema tunakwenda
kuonana na wananchi, itoshe kusema mwambao wote wa Pwani tutaugusa tutakutana
taifa zima," alisema Mbowe.
Azimio lingine la
Kamati Kuu kwa mujibu wa Mbowe ni kufutwa kwa mkataba huo na alisisitiza, chama
hicho kitafanya kila namna kuhakikisha Serikali inalitekeleza hilo.
"Msimamo wa
Chadema ni kwamba mkataba huu ufutwe wote, aidha tutatumia njia mbalimbali
ndani na nje ya nchi kuhakikisha mkataba unafutwa na maslahi ya nchi
yanalindwa," alisema.
Mbali na kufutwa
mkataba, Mbowe alisema kamati kuu hiyo iliazimia Bunge lifute azimio lake la
kuridhia mkataba huo kwa kuwa hauna maslahi kwa nchi.
Alieleza kamati kuu
iliazimia Serikali iwachukulie hatua kwa mujibu wa sheria, watu wote
walioshiriki kuingiza nchi katika mkataba huo usiorekebishika na
unaolidhalilisha Taifa.
"Kamati Kuu
inaunga mkono jitihada mbalimbali za wananchi kupinga mkataba huo, ikiwemo
walioamua kufungua kesi katika mahakama," alisema Mbowe.
Maazimio mengine ni
kushirikiana na wananchi bila kujali itikadi zao katika kupinga mkataba huo na
kuwahimiza kuona haja ya kudai Katiba Mpya.
"Ikiwa Bunge na
Serikali hazitachukua hatua, Chadema itaanzisha na kuhamasisha umma kuchukua
hatua kali dhidi ya Serikali hadi itakapochukua hatua," alisema.
Alieleza kamati kuu
hiyo imeridhika kuwa mkataba huo unakwenda kinyume cha Katiba na sheria za nchi
na kimataifa na umesababisha Serikali kuwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko
ya sheria ya kumiliki maliasili za nchi.
"Kamati Kuu
imejiridhisha kuwa hakuna utafiti wa kisayansi na uliochapishwa kwa umma
kuthibitisha ufanisi duni wa bandari zetu na ubora wa DP World, bali kila kitu
kilifanywa kwa siri," alisema. Uamuzi wa CCM
Julai 9 mwaka huu,
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) ilipokea na kujadili kwa kina
taarifa ya makubaliano hayo na kutoka na maazimio kuwa uwekezaji na uendeshaji
wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi. Taarifa ya CCM iliyotolewa na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Sophia Mjema ilieleza kikao cha NEC
chini ya uenyekiti wa Rais Samia kilikubaliana, Serikali iendelee kutoa elimu
kwa wananchi katika jambo hilo.
"Serikali iongeze
kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya
uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari," alisema Mjema na kuongeza:
“Serikali ihakikishe maoni chanya yenye tija, ya wananchi yanasikilizwa.”
…ni mjadala wenye afya
Jana, akizungumzia
suala hilo kwenye warsha ya kuwajengea uwezo waandishi na wahariri juu ya
masuala ya ukatili wa kijinsia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Damas Ndumbaru alisema mjadala unaoendelea nchi hivi sasa ni afya
kwa Taifa.
Lakini ameonya watu
wasiitumie vibaya Ibara ya 18 ya Katiba inayozungumzia uhuru wa kujieleza na
kutoa maoni.
"Huu utashi
alionao Rais (Samia) wa kutamani kuona watu wakizungumza, wakitoa maoni,
usigeuzwe kuwa mapambano ya watu kutukanana na kutweza wengine," alisema
Dk Ndumbaro ambaye kitalamu ni mwanasheria
Hata hivyo, alishangaa
kuona suala la bandari likijadiliwa kwa jazba na nguvu kama ndiyo mkataba wa
kwanza wa aina hiyo kwa nchi kusaini.
"Mbona tumesaini
mkataba kama huo kwenye mradi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima Uganda
na ardhi imetwaliwa kwa ajili ya mradi huo, mbona hatusemi nchi imeuzwa na watu
wamelipwa fidia!
"Nadhani kuna
haja ya kulijadili hili kwa hekima ili tufikie malengo ya mafanikio
tunayoyatamani badala ya kuendelea kutoleana maneno ya kashfa," alisema
Alisema ukisikiliza
mjadala mzima, hakuna mtu anayepinga uwekezaji bandari, ila wanalalamikia
baadhi ya vifungu wakitaka virekebishwe jambo ambalo Serikali imekubali
kuyapokea maoni hayo na itakwenda kufanyia kazi.
Alisema dhamira ya
Serikali ya kutaka uwekezaji bandarini ni njema na watu waondoe dhana ya kuwa
Rais ameamua kuiuza nchi.
Alisema cha msingi
kinachopaswa kufanywa ni kujadili na kuonyesha vifungu vyenye upungufu
vifanyiwe kazi na mambo mengine yaendelee.
Na:- Baraka Loshilaa
& Juma Issihaka #Mwananchi © 2023 |